Adili hilo halichanganyikani na woga unaomzuia mtu asitende inavyotakiwa, wala na ujanja unaotumia undumakuwili na ulaghai.
Kwa Kilatini inaitwa «auriga virtutum – dreva wa maadili», kwa kuwa inatakiwa kuongoza utekelezaji wa maadili mengine yote ikiyaonyesha kanuni na kiasi. Busara ndiyo inayoongoza uamuzi wa dhamiri. Mwenye busara anatenda kufuatana na uamuzi huo. Kwa njia ya busara tunatumia kwa hakika misimamo ya kiadili katika nafasi mbalimbali na kuondoa wasiwasi kuhusu la kutenda[3].
Katika Ukristo
Yesu aliitaja busara mara kadhaa, kwa kuwa inahitajiwa na wote ili wajiongoze vizuri, lakini inawafaa hasa wanaotakiwa kushauri au kuongoza wengine. Ila tuielewe vema, tusije tukaichanganya na vilema vinavyofanana nayo.
Kasoro za kuepwa
Tunatambua zaidi thamani ya adili fulani tukizingatia madhara ya vilema vinavyopingana nalo, ambayo mara nyingi ni ya wazi. Injili inaonyesha matokeo ya kutofikiria yakilinganisha wanawali wenye busara na wale wapumbavu (taz. Math 25:1-13). Mtume Paulo alisifu busara ya wazee, hasa waliowekwa juu ya jumuia za Kikristo, akiongeza tusiwe “watu wa kujivunia akili” (Rom 12:16) kwa sababu Mungu ataharibu “hekima yao wenye hekima” na kukataa “akili zao wenye akili” (1Kor 1:19) wanaotegemea uwezo na ujanja wao. Yesu alisali, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga” (Math 11:25).
Basi, tuepe kasoro mbili zinazopingana: upande mmoja kutofikiria, uzembe katika kuzingatia la kufanya, uamuzi wa harakaharaka; upande mwingine busara bandia, “nia ya mwili” (Rom 8:6), ambayo si adili, ina malengo ya kidunia tu, na mbinu nyingi za kujipatia faida: kwa kufanya hivyo wajanja hawataingia ufalme wa mbinguni.
Busara na kujitawala kadiri ya Augustino na Thoma wa Akwino
Inafafanuliwa kama akili nyofu inayoongoza matendo. Inaitwa dreva wa maadili ya kiutu, kwa kuwa linaratibu matendo ya haki, nguvu na kiasi na maadili mengine yanayotokana nayo, ikipanga kipimo cha kufuata, bila kuzidisha wala kupunguza. Lakini ili ipime vizuri inahitaji maadili hayo mbalimbali yawepo tayari, kama vile dreva wa gari la kukokotwa anavyohitaji farasi waliozoeshwa vizuri. Adili dreva na mengine yanahusiana pande zote na kustawi pamoja. Hakuna mtu anayeweza kuwa na busara asipokuwa na haki, nguvu, kiasi, uaminifu na utaratibu kulingana nayo, kwa sababu “kila mmoja anapima la kufanya kwa kufuata misimamo ya ndani ya utashi wake na hisi zake” (Thoma wa Akwino): mwenye kiburi anaona ni jema lile linalopendeza kiburi chake, kumbe mwadilifu anapenda kutenda mema bila kujulikana. Basi, “uamuzi wa busara ni wa kweli kiutendaji kadiri unavyolingana na unyofu wa utashi” (Thoma wa Akwino). Tena, busara haitakiwi tu kupima vizuri, bali pia kuagiza kwa nguvu matendo maadilifu; lakini haiwezi kufanya hivyo utashi usiponyoshwa na maadili hayo. Unyofu huo ni mzuri; kumbe mara nyingi siasa inazingatia faida tu, badala ya uadilifu, ikiacha yatendeke maovu makubwa bila kutetea haki za wanyonge hata kupatwa na matokeo ya kutisha. Kwa kufidia maovu hayo yanahitajika maisha matakatifu ya watu kadhaa ambao kwa ajili yao Mungu anaweza akatumia huruma kama kwa wale kumi “wenye haki” (Mwa 19:16-33).
Basi, aliyetenda dhambi ya mauti dhidi ya adili lolote, hawezi kuwa na busara yenye msimamo, kwa sababu utashi wake umepotoka kuhusu lengo kuu. Ni lazima tumpende Mungu kuliko nafsi yetu ili busara iwe na msimamo na kushikamana na maadili mengine ya kiutu. Hapo itatushauri mengi yanayojulikana na akili, itatukinga na matendo yasiyofikiriwa, itatawala silika yetu, itatuambia tusifuate ndoto za mchana wala tamaa za hisi, itatukumbusha wajibu wa kupokea mashauri ya watu wenye mwanga na mang’amuzi kuliko sisi, na wa kutii wanaotuongoza.
Adili hilo, kubwa kuliko yale yote linayoyaongoza, haliishii kutuzuia tusitende (hasa makuu) kwa kuogopa usumbufu na ugumu. Hiyo ni “busara” ya wasio na moyo wanaoyumbayumba daima kati ya mema na mabaya, watu vuguvugu wanaojitetea kwa kusisitiza wazo lao kuu, kwamba “tusizidishe”. Kumbe, adili la busara linaelekeza kutenda namna na wakati wa kufaa, bila kusahau lengo lipitalo maumbile, wala ari kwa utukufu wa Mungu na wokovu wa watu.
Mwanzoni mwa malezi maadili ya unyenyekevu, usafi wa moyo na uvumilivu yanasisitizwa kuliko busara, kwa sababu yanamuelekeza aliye nayo aamue vizuri kuhusu maisha ya Kiroho. Lakini baadaye, anapoanza kujiongoza katika mengi na kushauri wengine, anatakiwa kuzingatia madai ya busara asiamue harakaharaka. Hapo tunazidi kuelewa ukuu wa adili la Kikristo la busara linalokuja mara chini ya yale ya Kimungu na kuingiza mwanga wa maadili hayo katika yale ya kiutu.
Basi, busara ya Kikristo inatakiwa kustawi pamoja na upendo, na mitazamo yake ipitayo maumbile inatakiwa kushinda zaidi na zaidi mitazamo ya “akili ya chini” (Augustino). Lakini busara hiyo ya juu ni ya nadra. Zinafika nyakati, kama za dhuluma, ambapo upungufu wa mitazamo ya kawaida unaonekana wazi. Busara halisi haisahau kamwe ukuu wa lengo tunalopaswa kulielekea, bali inapima kila tendo kulingana na uzima wa milele, si kulingana na desturi za mazingira tunamoishi. Inakumbuka daima kile ambacho peke yake ni cha lazima. Ikisaidiwa na kipaji cha shauri, inakuwa upambanuzi mtakatifu unaopima yote kwa kipimo cha Mungu.
Upambanuzi huo unadai kwanza imani kubwa. Busara hairatibu matendo ya maadili ya Kimungu, kwa sababu ni makuu zaidi na kanuni yake ni Mungu mwenyewe: hayategemei kilele kilicho katikati ya vilema viwili vinavyopingana mabondeni na ambacho kinaonyeshwa na busara. Hata hivyo utekelezaji wa maadili ya Kimungu haufanyiki pasipo busara ambayo ionyeshe, k.mf. lini inafaa kusema juu ya imani, ama kutekeleza tendo hili au hili la upendo. Basi, busara ya Kikristo pamoja na upendo vinashikamanisha maadili yote.
Busara hiyo ikiangazwa na uvuvio maalumu wa kipaji cha shauri, kinachohusiana nayo, inapatana na unyofu wa njiwa alivyodai Bwana. Unyofu huo kamili si ujinga, unatunza siri zisizotakiwa kutobolewa usiongope kamwe. Kipaji cha shauri kinasaidia busara hasa katika nafasi ngumu zisizotarajiwa, ili kulinganisha katika neno au tendo moja maadili yanayoonekana kupingana, k.mf. usemakweli na uaminifu wa kutunza siri.
Kipaji hicho kinahusiana na heri ya wenye huruma kwa sababu mbili. Kwanza, tunatakiwa kuwa na huruma tuweze kushauri vilivyo wanaohitaji msaada huo, tuwainue kwa nguvu na upole bila kuwachukiza. Pili, busara inaposita kati ya ukali wa haki na haja ya kutosahau kamwe huruma, kipaji cha shauri kwa kawaida kinatuelekeza kwenye huruma ambayo itamuinua mkosefu na kumrudisha katika utaratibu wa haki, arekebishe alichoharibu kwa kujuta kwa dhati kuliko kwa kuvumilia adhabu pasipo upendo.
Tunaweza kuona zaidi ukuu wa busara ya Kikristo tuzingatia unyofu unaotakiwa kuendana nayo daima kadiri ya maneno ya Yesu: “Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote” (Math 24:45-47). Hayo yanahusu kwa namna ya pekee wale ambao wanatakiwa kuongoza wengine, na ambao watapata tuzo kuu: “Walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele” (Dan 12:3).
Busara ya kishujaa
Hiyo inazungumziwa kidogo, lakini katika nafasi ngumu busara pia inakuwa ya kishujaa. Adili hilo linahusu utekelezaji wa ukweli, yaani ukweli katika matendo. Ndiyo sababu Bwana alisema, “Iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua” (Math 10:16). Si rahisi kulinganisha kila mara maadili hayo, lakini yote mawili ni ya lazima kwa Mkristo anayetakiwa si tu kuwa mwadilifu kamili, bali kutenda daima kama mwana wa Mungu, akimtegemea kikamilifu na kuzidi kujua anavyomtegemea. Busara ya Kikristo katika ngazi ya juu inajua wazi mema yanayompasa mtoto wa Mungu, na inaelekeza kwa imara maadili mengine yayatende kitakatifu. Wanaolenga ukamilifu wanatakiwa kulenga maadili yote kwa ngazi ya juu, jambo linalodai kiwango hichohicho cha busara walau kuhusu utakatifu wao wenyewe. Adili hilo ni la lazima zaidi kwa wale wanaopaswa kushauri na kuongoza wengine.
Tunapoiamini mno busara yetu, Mungu akitaka kututakasa anatuacha tuangukie makosa ya wazi, au tusahau au kutozingatia mambo, na matokeo yake yanatuaibisha. Baada ya takaso hilo busara inaweza ikawa ya kishujaa na kuongozana na kiwango cha juu cha kipaji cha shauri ambacho tunapokea uvuvio wa Kimungu wa kuhisi la kufanya katika nafasi ngumu.
Inatokea vile Bwana anapomfanya mtumishi wake atende namna ambazo wengi wanaona hazina busara, k.mf. Fransisko wa Asizi katika kupenda ufukara. Ndivyo walivyofanya wale wote ambao kwa uvuvio wa Mungu walikabili kazi ngumu zaidi, kama kuokoa makahaba au majambazi hata kuwafanya watawa; hapo walijikuta katika nafasi ambapo kutenda na kutotenda kulionekana vilevile kukosa busara, hata iliwapasa kumuomba Bwana uvuvio wa kipaji cha shauri, pamoja na kutulia mikononi mwake. Busara kamili haitenganiki na sala ya kudumu kwa kupata mwanga wa Mungu; vilevile inaelekeza kusikiliza mashauri mazuri ya wanaoweza kutuangazia na inadhihirisha ukomavu wa roho.
Kuhusu mambo ya pekee yapitayo maumbile, busara halisi inachukua tahadhari: haiyakanushi kimsingi, bali inayapima na kuyatolea tamko pale tu inapolazimika na baada ya kumuomba Mungu mwanga. Busara hiyo ya hali ya juu inadhihirika pia katika kupima miito ya pekee. Ushujaa wa adili hilo unadhihirika hasa katika matendo ambayo binadamu anayaona hayana busara, kumbe matokeo yake yanakuja kuonyesha yalivyokuwa na busara ya juu. Ndivyo Mwokozi alivyowatuma mitume wakekumi na wawili waongoe ulimwengu bila chombo chochote cha kibinadamu.
↑"Integral parts" of virtues, in Scholastic philosophy, are the elements that must be present for any complete or perfect act of the virtue. The following are the integral parts of prudence:
Memoria : accurate memory; that is, memory that is true to reality; an ability to learn from experience;
Docilitas : an open-mindedness that recognizes variety and is able to seek and make use of the experience and authority of others;