Vyombo vya anga vinaundwa kwa kazi nyingi pamoja na mawasiliano, kubeba vifaa vya kutazama dunia au hali ya hewa, kufanyia utafitisayari nyingine au kusafirisha watu na mizigo.
Vyombo vingine vinaingia kwa muda mfupi tu juu ya angahewa bila kumaliza mzingo wa dunia. Vingine vinazunguka kwenye mzingo kwa muda mrefu hata miaka.
Chombo cha angani cha kwanza kilikuwa Sputnik 1 kilichorushwa na Umoja wa Kisovyeti mwaka 1957 na kuzunguka dunia kwa miezi 3. Kilifuatwa na chombo cha Marekani "Explorer 1" mwaka 1958.
Ilhali maandalizi ya safari za kupeleka watu anga-nje ni ghali sana bila kuleta faida kubwa kiuchumi au kisayansi, kuna mamia ya vyombo vya anga vinavyozunguka dunia na kutekeleza kazi muhimu. Hivi huitwa pia satelaiti zikifuata mwendo wa kudumu wa kuzunguka dunia au kukaa mahali pamoja angani juu ya uso wa dunia. Utabiri wa hali ya hewa hutegemea data na picha kutoka vyomboanga. Sehemu ya majadiliano kwa simu na sehemu kubwa ya picha za televisheni hupitia satelaiti, na vilevile data za teknolojia kama GPS.
Vyomboanga vingine kama vipimaanga vinapewa kazi ya upelelezi angani hasa kukaribia sayari, kukusanya data zao na kuzituma duniani. Habari nyingi juu ya sayari za mfumo wa jua letu zimepatikana kutokana na upimaji uliotekelezwa na vipimaanga hivi.