Hivyo Kiarabu ni mojawapo ya lugha muhimu sana duniani ikisomwa kwa viwango tofauti na mamilioni ya waumini Waislamu wakielekea kujifunza na kuelewa kitabu cha Korani. Kama lugha ya kidini ina athari na taathira kubwa juu ya lugha nyingi ulimwenguni na juu ya ustaarabu na utamaduni wa watu na makabila tofautitofauti walio Waislamu.
Ni lugha iliyokusanya aina nyingi za mithali na mafumbo, na ina utamaduni mkubwa wa nyimbo, mashairi na misemo, nayo inakubaliwa na watu wengi duniani kuwa lugha yenye utamu wa matamshi na uzuri wa lafudhi.
Kwa kuwa Qurani Tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad na Mashairi ya zama za Ujahili ndio yenye kudhibiti lugha hii isitetereke wala kubadilika na kupotea kama lugha nyingine nyingi, leo, baada ya miaka zaidi ya elfu, imebaki thabiti kama ilivyokuwa wakati ilipoandikwa Qurani, na mabadiliko yoyote yaliyotokea hayana uhusiano na lugha yenyewe ya Kiarabu, bali yana uhusiano na lahaja na vilugha mbalimbali zinazotumika na Waarabu wa sehemu fulani ya nchi au mji. Ama lugha rasmi ya Kiarabu basi imedhibitika kulingana na Qurani na Sunnah, ili maandishi hayo yaendelee kufahamika milele.
Umuhimu wa lugha hii unazidi kukua kila siku kwa sababu ya kutumika kwenye maeneo ya katikati ya ulimwengu baina ya mabara ya kale (Afrika, Asia na Ulaya) na mabara mapya ya ulimwengu (Amerika ya Kaskazini na Kusini).
Asili ya lugha ya Kiarabu
Kiarabu, pamoja na lugha ya Kiebrania (ya Uyahudi) na Kiaramu (ya Mashariki ya Kati) na Kiamhari (ya Ethiopia) zinatokana na asili moja ya lugha ya Kisemiti. Kuna lugha nyingi vile vile ambazo zinatokana na asili hii, kama Kiashuri, Kifinisia, Kibabili na kadhalika. Baadhi ya hizi lugha zimekufa au kuwa na wazungumzaji wachache, na kwa hiyo umuhimu wake umekuwa si mkubwa kama ulivyo umuhimu wa lugha ya Kiarabu.
Kiarabu Fasihi ambacho kilikuwa kikitumika zama za Ujahili kabla ya kuja Uislamu, na kuendelea kutumika baada ya kuja Uislamu katika Qurani na Sunnah za Mtume Muhammad,
Kiarabu Mamboleo ambacho kinatumika katika maandishi na mazungumzo rasmi baina ya Waarabu wote kwa jumla, na
Kiarabu Lahaja ambacho kinatumika na watu maalumu katika sehemu fulani za nchi au vijiji, na ni lugha ya mahali tu, kama vile Kiyemeni au Kimasri au Kishami au Kimaghribi, na lugha hizi au lahaja hizi zinakuwa zinatofautiana sana baina yake katika misamiati na matumizi.
Kiarabu fasihi
Kiarabu ni lugha ya zamani sana (tarehe yake inarudi nyuma zaidi ya miaka 2000), nayo pamoja na lugha nyinginezo za Kisemiti zilikuwa zikitumika katika nchi za Mashariki ya Kati. Kiarabu Fasihi ilianza kuwa na nguvu zaidi baada ya kuteremshwa Qurani kwa lugha hiyo na kuhifadhiwa Hadithi za Mtume Muhammad na kuwa ndio chanzo cha lugha zote nyinginezo za Kiarabu zilizokuweko wakati huo.
Maandishi mengine ya Kiarabu yaliyokuwa muhimu sana ni maandiko ya falsafa na sayansi. Waarabu walitafsiri maandiko ya Wagiriki wa Kale wakaendeleza ujuzi wao. Katika karne zilizopita Ulaya ilipokea sehemu kubwa ya elimu yake kutoka kwa Waarabu kwa njia hiyo.