Idadi ya watu kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 ilikuwa 61,741,120[2], (nchi ya 24 duniani) kutoka 44,928,923 waliohesabiwa katika sensa ya mwaka 2012, likiwa ongezeko la 3.2% kwa mwaka.
Msongamano ni wa watu 47.5 kwa km² (nchi ya 124 duniani).
Jina "Tanzania" liliundwa kama mkusanyiko wa majina ya maeneo mawili yaliyoungana kuunda nchi: Tanganyika na Zanzibar.[6] Jina lilipatikana kwa mashindano yaliyotangazwa mwaka 1964 na serikali kutafuta jina fupi zaidi kuliko "Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar".
Mshindi alikuwa mwenyeji wa Dar es Salaam aliyeitwa Mohamed Iqbal Dar[7]. Alipendekeza kuunganisha herufi tatu za kwanza za TANganyika na ZANzibar akafikia "Tanzan". Hakuridhika bado, akaona nchi nyingi za Afrika zina majina yanayoishia na "ia" akaongeza herufi hizi. Mwenyewe alieleza baadaye chaguo lake kwamba aliamua kutumia "I" ya jina lake Iqbal na "A" ya jina la dhehebu lake analolifuata katika Uislamu la Ahmadiyya.[8]
Jina "Tanganyika" linatokana na maneno ya Kiswahili "tanga" na "nyika", yakiunda msemo "tanga nyikani". Wakati fulani inaelezwa kama marejeleo ya Ziwa Tanganyika. [9] Jina la Zanzibar linatokana na "zenji", jina la watu wa eneo hilo (inadaiwa lina maana ya "nyeusi"), na neno la Kiarabu "barr", ambalo linamaanisha pwani au ufukwe.[10]
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (1995–2005) aliendeleza mfumo wa uchumi wa soko huria ambapo mashirika ya umma yalibinafsishwa.
Tarehe 21 Desemba2005Jakaya Kikwete aliapishwa kuwa Rais wa nne wa taifa (2005–2015), naye aliendeleza sera za watangulizi wake akitokea chama hichohicho cha CCM.
Tarehe 5 Novemba 2015 aliapishwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli (wa CCM vilevile).
Ikiwa na eneo la kilomita za mraba 947,303 (365,756 sq mi), Tanzania ni nchi ya 13 kwa ukubwa barani Afrika na ya 31 kwa ukubwa duniani.[11] Inapakana na Kenya na Uganda upande wa kaskazini; Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo upande wa magharibi; na Zambia, Malawi, na Msumbiji upande wa kusini.
Tanzania iko kwenye pwani ya mashariki ya Afrika na ina ufuo wa Bahari ya Hindi takriban kilomita 424 (885 mi).[12] Pia inajumuisha visiwa kadhaa vya pwani, vikiwemo Unguja (Zanzibar), Pemba, na Mafia. Tanzania ni nchi yenye sehemu za juu na za chini kabisa barani Afrika: Mlima Kilimanjaro, wenye urefu wa mita 5,895 (futi 19,341) juu ya usawa wa bahari, na kina cha Ziwa Tanganyika, katika mita 1,471 (futi 4,826) chini ya usawa wa bahari kwa mtiririko huo.
Tanzania ina milima na misitu minene kaskazini-mashariki, ambako kuna Mlima Kilimanjaro. Nchi iko katika eneo la Maziwa makubwa ya Afrika, hivyo maziwa yanafunika km2 61,500, yaani 6% za eneo lote la nchi. Upande wa kaskazini na magharibi kuna Ziwa Victoria, ziwa kubwa zaidi barani Afrika, na Ziwa Tanganyika, ziwa lenye kina kirefu zaidi barani humo, linalojulikana kwa aina yake ya kipekee ya samaki. Upande wa kusini magharibi kuna Ziwa Nyasa. Eneo la katikati mwa Tanzania ni uwanda mkubwa, wenye tambarare na ardhi ya kilimo. Ukanda wa mashariki una joto na unyevunyevu, huku Visiwa vya Zanzibar vikiwa karibu. Maporomoko ya maji ya Kalambo katika mkoa wa kusini-magharibi mwa Rukwa ni maporomoko ya pili kwa urefu barani Afrika, na yanapatikana karibu na ufuo wa kusini-mashariki wa Ziwa Tanganyika kwenye mpaka na Zambia. [13] Eneo la Hifadhi ya Menai Bay visiwani Zanzibar ndilo eneo kubwa zaidi la bahari lililohifadhiwa.
Hali ya hewa inatofautiana sana ndani ya Tanzania. Katika nyanda za juu, halijoto huanzia 10 hadi 20 °C (50 na 68 °F) wakati wa msimu wa baridi na joto kwa mtiririko huo.
Tanzania hupata majira ya joto katika miezi ya Desemba, Januari na Februari (25–31 °C au 77.0–87.8 °F) huku kipindi cha baridi zaidi kikitokea kati ya Mei na Agosti (15–20 °C au 59–68 °F). Halijoto ya kila mwaka ni 20 °C (68.0 °F).
Hali ya hewa ni baridi katika maeneo ya milima mirefu. Tanzania ina vipindi viwili vikuu vya mvua: mvua za vuli hunyesha katika miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba na mvua za masika hunyesha katika miezi ya Machi, Aprili na Mei ingawa zipo tofauti ndogo kati ya sehemu mbalimbali.[14] Kiasi cha mvua na halijoto husababisha tofauti za aina ya uoto wa asili, udongo na aina ya mazao yanayolimwa.
Mabadiliko ya hali ya hewa nchini Tanzania yanasababisha kuongezeka kwa joto na uwezekano mkubwa wa matukio ya mvua kubwa (kusababisha mafuriko) na vipindi vya ukame.[15][16] Mabadiliko ya hali ya hewa tayari yanaathiri sekta za kilimo, rasilimali za maji, afya na nishati nchini Tanzania. Kupanda kwa kina cha bahari na mabadiliko ya ubora wa maji kunatarajiwa kuathiri uvuvi na ufugaji wa samaki.[17]
Tanzania ina takriban 20% ya spishi za wanyama wengi wa Afrika wenye damu moto, wanapatikana kwenye mbuga zake za Taifa, hifadhi na bahari. Hifadhi za Taifa na mbuga za wanyama zimeenea katika eneo la zaidi ya kilomita za mraba 42,000 (sq. mi 16,000) na kuunda karibu 38% ya eneo la nchi.[19][20] Tanzania ina mbuga 21 za taifa, pamoja na hifadhi mbalimbali za wanyamapori na misitu, ikijumuisha Hifadhi ya Ngorongoro. Magharibi mwa Tanzania, Hifadhi ya Taifa ya Gombe ni kitovu ya uchunguzi unaoendelea wa Jane Goodall wa tabia ya sokwe, ambao ulianza mwaka wa 1960.[21][22]
Tanzania ina bioanuwai nyingi na ina aina mbalimbali za makazi ya wanyama.[23] Katika uwanda wa Serengeti nchini Tanzania, nyumbu (Connochaetes taurinus mearnsi), "bovids" wengine na pundamilia[24] hushiriki katika uhamaji mkubwa wa kila mwaka. Tanzania ni nyumbani kwa takriban spishi 130 za amfibia na zaidi ya spishi 275 za wanyama watambaao, wengi wao wanapatikana Tanzania tu na wamejumuishwa katika orodha ya International Union for Conservation of Nature.[25] Tanzania ina idadi kubwa ya simba duniani.[26]
Tangu uhuru, mgawanyo wa madaraka na uhusiano miongoni mwa mihimili hiyo uliimarishwa kwa kuzingatia wakati, mahitaji ya demokrasia na misingi ya utawala bora na umeainishwa pia katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 4 (1).
Kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi pia kulikuwa hatua ya kuendelea kuimarisha utawala wa ushiriki wa wananchi kadiri mahitaji ya upanuzi wa maono na falsafaduniani.
Ugatuzi, yaani mgawanyo wa kiutawala, unafuata Katiba ya nchi I 2.2. Tanzania imegawiwa kwa mikoa 31. Kila mkoa huwa na wilaya ndani yake. Jumla ya wilaya ni 169, ambazo kati yake 34 ni miji.
Watu wa Tanzania hawaenei sawasawa. Katika maeneo makavu sana, kwa wastani kuna mtu mmoja tu kwa kilomita ya mraba (1/km²), lakini sehemu zenye rutuba za bara, kuna watu 51 kwa kila kilomita ya mraba. Hatimaye huku Unguja kuna watu 134 kwa kilomita ya mraba na katika Mkoa wa Dar es Salaam ni 3,133 kwa kilomita ya mraba.
Asilimia 70 hivi huishi vijijini, ingawa uhamiaji mijini unakwenda kasi.[28]
Makabila
Jamii nyingi za watu zimeishi na kushirikiana katika eneo la Tanzania bara kwa milenia nyingi.
Kati ya jamii hizo, nyingi zilikuja kutoka maeneo mengine ya Afrika.
Nyingi katika jamii zilizohamia sehemu hii ziliingia katika makundi madogomadogo kwa amani, ingawa ziko zilizoingia kwa njia ya uvamizi na vita. Baadhi ya jamii zilizovamiwa zilijihami na kuwazuia wahamiaji wasiendelee kuteka maeneo mengine.
Kufikia mwaka 1884, wakati Wajerumani walipoanza harakati za kufanya sehemu hii ya Afrika kuwa koloni lao, kulikuwa na makabila zaidi ya 120 katika eneo la Tanzania bara.
Jambo la pekee kuhusu jamii zilizoishi na zinazoendelea kuishi Tanzania ni kwamba wakazi asili wanawakilisha makundi yote makuu manne ya lugha barani Afrika.[29]
1. Idadi kubwa sana ya Watanzania ni wa jamii ya Wabantu (k.m. Wazaramo, Wapare na Wapogoro).
Nchini Tanzania kuna lugha za kikabila zaidi ya mia moja na ishirini, kwa kuwa kila kabila lina lugha yake.
Kiswahili ndiyo lugha ya taifa na inazidi kuwa lugha mama[30] kwa watoto wengi, hasa mijini.[31] Walau asilimia 90 za wakazi wanakitumia walau kama lugha ya pili. Kiswahili ni mojawapo kati ya lugha za Kibantu: hii imesaidia sana kukubaliwa kwa Kiswahili nchini, kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania ni wasemaji wa lugha za Kibantu. Kiswahili kinatumika kama lugha baina ya watu wa makabila mbalimbali na kwa mambo rasmi; kwa hiyo ni lugha rasmi ya dhati.
Baada ya uhuru, Kiingereza (iliyokuwa lugha ya kikoloni kabla ya uhuru) iliendelea kutumika kwa mambo kadhaa rasmi na kwa elimu kuanzia sekondari ingawa sera mpya inataka Kiswahili kishike nafasi yake hadi chuo kikuu;[32] kwa hiyo ilichukuliwa kama lugha rasmi ya dhati pamoja na Kiswahili. Lakini utumizi rasmi wa Kiingereza umepungua katika milongo iliyopita, na sasa utumizi huu karibu umekwisha. Kwa hiyo siku hizi ni kawaida zaidi kuchukulia Kiswahili kama lugha rasmi ya dhati pekee.
Nchi haina dini rasmi na katiba ya Tanzania inatangaza uhuru wa dini kwa wote. Mara nyingi idadi ya wafuasi wa dini hutajwa kuwa theluthi moja Waislamu, theluthi moja Wakristo na theluthi moja wafuasi wa dini za jadi. Lakini tangu uhuru swali la dini ya wananchi halijaulizwa tena katika sensa, kwa hiyo kadirio la theluthi-theluthi inawezekana ni zaidi azimio la kisiasa.
Kwenye funguvisiwa la Zanzibar idadi ya Waislamu huaminiwa kuwa takriban 97%.
Hadi sasa idadi ya barabara za lami si kubwa. Kuna hasa njia nzuri kati ya Dar es Salaam, Mbeya katika kusini-magharibi, Dodoma katika kitovu cha nchi, Arusha / Tanga katika kaskazini-mashariki. Kusini-Mashariki na Magharibi ya nchi kwa jumla haina barabara nzuri na mawasiliano ni magumu.
Mashirika mawili ya reli yanayohudumia Tanzania: ni TRC (Shirika ya Reli Tanzania - Tanzania Railways Corporation) na TAZARA (Tanzania-Zambia Railways Corporation). TRC imetawala reli ya kati kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma halafu reli ya Tanga kati ya Tanga na Arusha. Tazara imeunganisha Dar es Salaam na kusini ya nchi hadi Zambia. Zote hazikutunzwa vizuri na usafiri unakumbwa na huduma mbaya pamoja na ajali.
Huduma kwa ndege zinatumia hasa viwanja vya ndege 11 vyenye barabara ya lami kwa ajili ya ndege, hasa Julius Nyerere/Dar es Salaam, Kilimanjaro/Arusha-Moshi na Zanzibar-Kisauni. Pia kuna viwanja vingine vya ndege kama vile uwanja wa ndege wa Mwanza, Bukoba na Kigoma.
Usafiri wa majini pia unafanyika hasa katika bahari ya Hindi, ingawa hakuna meli ya serikali hapo na mashirika binafsi hutoa huduma. Usafiri wa majini hufanyika pia katika maziwa ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa. Miongoni mwa meli ni MV Bukoba iliyozama tarehe 21 Mei1996 pamoja na abiria karibu 1,000 na MV Nyerere iliyozama tarehe 20 Septemba2018 pamoja na abiria zaidi ya 200.
Katika ziwa Tanganyika ipo meli ya Mv Liemba ambayo ilianza kutumika tangia kipindi cha ukoloni wa Wajerumani: inatoa huduma kati ya miji ya mwambao wa ziwa Tanganyika na nchi jirani.
Mwaka 2017 ulianza ujenzi wa awamu ya kwanza ya njia ya geji sanifu nchini Tanzania inayolenga kuunganisha Dar es Salaam na Morogoro.[33] Njia hii inatarajiwa kuendelea hadi Mwanza na hatimaye hadi Burundi.
Urithi wa Dunia
Mahali pafuatapo katika Tanzania pamepokewa katika orodha ya UNESCO ya "Urithi wa Dunia" (mwaka wa kukubaliwa – jina la mahali)
Kuna aina zaidi ya tano za muziki nchini Tanzania, kama zilivyofafanuliwa na BASATA ni pamoja na ngoma(ngoma za asili), dansi, kwaya (muziki wa injili), taarab, na bongo flava (pop/hip hop).[34][35] Ngoma ni muziki wa dansi wa kitamaduni, ngoma hutofautiana kati ya kabila na kabila.[36][37] Dansi ni muziki wa bendi unatokana na muziki wa soukous kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (au "rumba ya kikongo").[38][39] Taarab ni muziki wa Waafrika wa pwani uliopokea athira kutoka tamaduni nyingi, hasa muziki wa Waarabu na Wahindi. Kimsingi ni uimbaji wa mashairi unaofuata muziki wa bendi.[40] Kwaya ni muziki ambao asili yake ni kanisani. Bongo flava ni muziki wa pop wa Tanzania uliozaliwa na muziki wa kizazi kipya, unajumuisha reggae, RnB, na hip hop, uliochanganywa na vionjo vya asili (flava) lakini tangu wakati huo umekua na kuwa muziki wa kipekee wa maeneo ya Maziwa Makuu.[41] Asili mbalimbali za ushawishi zimesaidia kufanya bongo flava kuwa muziki maarufu zaidi Afrika Mashariki, na muziki mmojawapo kati ya ile maarufu zaidi katika bara la Afrika.[42][43]
Tangu kuundwa kwa Tanzania hadi 1993, kurekodi na usambazaji wote wa muziki ulisimamiwa kikamilifu na BASATA, hasa kupitia Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD).[44] Ni aina 4 tu za muziki za Kitanzania zilizoruhusiwa kurekodiwa au kutangazwa, ambazo wakati huo zilikuwa ngoma, taarab, kwaya na dansi. Sheria ya Huduma za Utangazaji ya 1993 iliruhusu mitandao ya kibinafsi ya matangazo na studio za kurekodi.[45] Haya ni mojawapo ya mabadiliko muhimu zaidi katika tasnia ya muziki ya Tanzania tangu kuanzishwa kwa nchi miaka 30 kabla.[46] Miaka michache kabla ya Act ya 1993, muziki wa hip hop ulikuwa umeanza kuimarika katika miji ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza. Ilikuwa ikianza mageuzi kutoka kwenye hip hop ya Kiingereza huko Uzunguni, maeneo tajiri kama Oysterbay na Masaki pamoja na shule za kimataifa, hadi kizazi kipya Uswahilini, vitongoji maskini na kutumia Kiswahili.[47] Mara tu baada ya kufunguliwa kwa mawimbi ya redio, bongo flava ilizaliwa ikienea kwa haraka kote nchini, na katika Maziwa Makuu.[48]
Utamaduni wa kifasihi wa Tanzania kimsingi ni wa simulizi.[49]: 68 Tanzu na vipera maaarufu vya fasihi simulizi ni pamoja na ngano, mashairi, mafumbo, methali na nyimbo.[49]: 69 Sehemu kubwa zaidi ya fasihi simulizi iliyorekodiwa Tanzania ni ya Kiswahili, ingawa lugha za makabila ya Tanzania zina mapokeo yake ya simulizi. Fasihi simulizi ya nchi imekuwa ikipungua kwa sababu ya mabadiliko ya muundo wa jamii, na kufanya uwasilishaji wa fasihi simulizi kuwa mgumu zaidi, pia teknolojia za kisasa zinachangia kushushwa kwa thamani ya fasihi simulizi.[49]: 68–9
Baada ya kifo cha Tingatinga mwaka wa 1972, wasanii wengine walikubali na kuendeleza mtindo wake, na aina hiyo sasa ndiyo mtindo muhimu zaidi unaolenga utalii katika maeneo ya Afrika Mashariki.[49]: 113 [50]
Mchezo maarufu nchini Tanzania ni mpira wa miguu. Ingawa mpira wa miguu (kandanda) unaongoza kwa ufuasi mkubwa miongoni mwa vijana, michezo mingine kama vile mpira wa kikapu, mchezo wa ngumi na riadha inazidi kuwa maarufu miongoni mwa watu.[51][52] Baraza la Michezo la Taifa ndicho chombo kinachosimamia michezo nchini chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni.[53]
Tanzania ina tasnia maarufu ya filamu inayojulikana kwa jina la "Bongo Movie".[63] Studio nyingi za utayarishaji filamu za Kitanzania ziko Dar es Salaam.
↑Edoarado Razzetti and Charles Andekia Msuya (2002) "Introduction"Archived 16 Julai 2020 at the Wayback Machine, Field Guide to Amphibians and Reptiles of Arusha National Park. Tanzania National Parks. p. 11
↑Grantham, H. S.; na wenz. (2020). "Anthropogenic modification of forests means only 40% of remaining forests have high ecosystem integrity – Supplementary Material". Nature Communications. 11 (1): 5978. doi:10.1038/s41467-020-19493-3. ISSN2041-1723.
↑Ulrich Ammon; Norbert Dittmar; Klaus J. Mattheier (2006). Sociolinguistics: An International Handbook of the Science of Language and Society. Walter de Gruyter. pp. 1967–. ISBN 978-3-11-018418-1.
↑Kadiri ya Ulrich Ammon; Norbert Dittmar; Klaus J. Mattheier (2006). Sociolinguistics: An International Handbook of the Science of Language and Society. Walter de Gruyter. p. 1967. ISBN 978-3-11-018418-1 tayari Kiswahili ni lugha ya kwanza kwa asilimia 10 za wananchi
↑Concise Encyclopedia of Languages of the World. Elsevier. 2010. pp. 1026–. ISBN 978-0-08-087775-4.
↑"Tanzania Ditches English In Education Overhaul Plan". AFK Insider. 17 February 2015. Retrieved 23 February 2015.
↑"Hasheem Thabeet Stats". Basketball-Reference.com (kwa Kiingereza). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-12-07. Iliwekwa mnamo 2022-06-16.
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Tanzania kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.