Kwa Kiswahili cha kila siku mara nyingi hakuna tofauti kati ya Dunia na ulimwengu. Lakini kama lugha inataka kujadili habari kwa undani pamoja na ujuzi wa siku zetu kuna ulazima wa kutofautisha kati ya ngazi mbalimbali za mazingira tunamoishi.
Kwa maana hiyo Dunia ni hasa sayari tunapoishi. Zamani watu waliona Dunia kwa maana hiyo ni sawa na ulimwengu wote. Lakini maendeleo ya sayansi yametuonyesha upeo mkubwa zaidi uliopo ng'ambo ya sayari yetu na hata ng'ambo ya mfumo wa Jua letu na sayari zake. Kwa hiyo neno "ulimwengu" limekuwa muhimu kwa sababu linalenga kiasili kwa jumla la vitu vyote si kwa sayari yetu hasa.
Katika Wikipedia hii tunatumia neno "ulimwengu" kama Kiingerezauniverse au cosmos. "Dunia" tunatumia kwa maana ya Kiingereza earth. Wakati mwingine lugha za Ulaya zinatumia "universe" karibu sawa na "space" au "outer space" zikimaanisha nafasi kubwa ulimwenguni nje ya Dunia yetu. Hali halisi Dunia yetu ni ndogo sana ulimwenguni na kwa hiyo upeo wa "space" ni karibu sawa na upeo wa "universe". Lakini lugha nyingi zinatofautisha kati ya nafasi ile kubwa nje ya Dunia na dhana ya ulimwengu kama jumla ya vyote.
Kwa Kiswahili ni afadhali kutofautisha vilevile. Kwa kawaida tunatumia neno "anga" linalomaanisha kiasili kile kinachong'aa yaani mahali pa mwanga jinsi ilivyo anga juu yetu inayoangazwa na Jua. Kutokana na maana hiyo ya msingi "anga" linamaanisha yote ambayo ni juu yetu. Hivyo "anga" linataja mara nyingi angahewa ya Dunia, au yale ya buluu yanayoonekana juu yetu. Lakini hutumiwa pia kwa nafasi kubwa nje ya angahewa. Hapa tunatumia pia lugha ya "anga-nje" tukitaka kutofautisha angahewa na ule uwazi mkubwa kati ya nyota na galaksi.
Ulimwengu na sayansi
Ulimwengu hutazamiwa na matawi mbalimbali ya sayansi na utaalamu.
Astronomia ni sayansi inayotumia elimu ya fizikia na kemia kwa kutazama, kupima na kuchungulia vitu kwenye anga-nje. Mkono mmoja wa astronomia unaoshirikiana zaidi na falsafa ni kosmolojia inayoangalia hasa asili ya ulimwengu kulingana na kanuni asilia.
Mkono wa pekee ya biolojia inatafakari nafasi za uhai nje ya Dunia yetu kwa kushirikiana na astronomia.
Falsafa pamoja na sayansi mbalimbali inauliza maswali juu ya tabia na sifa za Dunia na matatizo ya kuitambua.
Theolojia pamoja na elimu ya kidini inatazama ulimwengu kama kazi ya Mungu inauliza maswali jinsi gani mapokeo ya kidini na maanddiko matakatifu yanalingana na mtazamo mpya wa sayansi juu ya ulimwengu.
Ukubwa na umri wa ulimwengu
Astronomia na kosmolojia zimekadiria umri na ukubwa wa ulimwengu jinsi ulivyo kuwa kubwa sana. Kwa kutumia kipimo cha mwakanuru kunakadiriwa ya kwamba ulimwengu una rediasi ya mwakanuru angalau bilioni 78.
Umri wa ulimwengu hukadiriwa kwa sasa kuwa miaka bilioni 13.7. Hesabu hii inaanza kwenye mlipuko mkuu wa asili ambayo ni nadharia inayotumiwa na wataalamu wengi.
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Ulimwengu kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.