Wamanda ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi katika Mkoa wa Njombe, Wilaya ya Ludewa. Pia wako katika Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Mbinga. Katika wilaya ya Ludewa Wamanda wanapatikana katika kata za Manda, Ruhuhu, Luilo, Iwela, Mkomang'ombe, Ludewa na Masasi. Katika mkoa wa Ruvuma wanapatikana zaidi kaskazini mwa wilaya ya Mbinga.
Wamanda kwa kiasi kikubwa wanaongea Kimanda, lugha yenye mchanganyiko wa Kingoni na Kinyasa kwa mawasiliano.
Wamanda walio wengi ni Wakristo wa madhehebu ya kianglikana na Kikatoliki. Kuna idadi ndogo sana ya Wamanda wanaoendelea kufuata dini asilia za Kiafrika. Hata hivyo, pamoja na kufuata Ukristo, Wamanda wengi bado wana mazoea ya kuendelea kuienzi mizimu na mahoka.
Wakati wa ukoloni na mara baada ya uhuru Wamanda wengi walifanikiwa kusoma na kuwa na elimu nzuri wakapata nafasi nzuri serikalini. Mfano wa Wamanda waliofanikiwa kufikia nafasi za juu nchini Tanzania ni pamoja na hayati Horace Kolimba, Crispin Mponda, na Valieth aliyekuwa mbunge wa kwanza wa wilaya ya Ludewa.
Kwa sasa kiwango cha elimu kwa Wamanda kipo chini sana kwa sababu mbalimbali, zikiwemo upungufu wa walimu katika shule za kata na hali ngumu ya uchumi inayosababisha wanafunzi wengi washindwe kumaliza japo kidato cha nne, au wakimaliza wanamaliza kwa madaraja ya chini sana, na hivyo kushindwa kuendelea, hata Wamanda wengi kwa sasa wakiondoka kwao, mara nyingi huwa wagumu mno kurudi kwao kwa kuwa kuna hali ngumu sana ya kiuchumi na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa hatari wa ukimwi.
Wilaya ya Ludewa, pamoja na kujaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa makaa ya mawe na chuma, wananchi wake bado wana hali mbaya ya kiuchumi na kwa ujumla Wamanda wanategemea misaada ya ndugu zao wanaoishi katika maeneo ya mijini kwa kiwango kikubwa.
Shughuli kuu za uchumi wa Wamanda ni pamoja na uvuvi wa samaki na ukulima wa mazao madogomadogo.
Chakula kikuu cha Wamanda ni ugali wa muhogo na samaki.
|
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wamanda kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
|