Mtu huyu anaitwa "dikteta" ingawa cheo rasmi mara nyingi ni "rais" au "kiongozi wa taifa". Wakati mwingine neno "udikteta" linataja hali ambayo kundi la watu linashika madaraka yale kwa pamoja, kwa mfano kamati ya wanajeshi waliochukua madaraka ya serikali.
Katika historia mfumo wa ufalme ambapo mfalme, sultani, kaisari au mtemi anashika madaraka yote peke yake kwa kawaida hauitwi udikteta. Lakini pale ambapo mfalme anapuuza katiba ya taifa na kutwaa madaraka ambayo si yake kikatiba anaweza kuitwa dikteta pia.
Udikteta wa kijeshi
Aina ya udikteta inayotokea mara kadhaa duniani ni udikteta wa kijeshi ambao viongozi wa jeshi wamechukua madaraka ya serikali kwa nguvu ya silaha zao. Hii ilikuwa njia hasa ya udikteta kuenea Afrika baada ya uhuru kwa sababu katika nchi nyingi za Afrika wanajeshi walipindua serikali na kutwaa madaraka kwa muda fulani.
Tabia za udikteta
Sheria na haki za binadamu
Kila nchi inahitaji sheria na pia udikteta hauwezi kuongoza bila sheria. Lakini tabia muhimu ya udikteta ni ya kwamba dikteta ana nafasi au uwezo wa kupuuza sheria au kufanya maazimio nje ya sheria na hakuna njia ya kumlazimisha kutii sheria.
Mara nyingi uhuru na haki za wananchi zimepunguzwa sana au kuondolewa kabisa kwenye mfumo wa udikteta. Kumbe tabia muhimu ya demokrasia ni mgawanyo wa madaraka na humo uhuru wa mahakama. Katika udikteta serikali inateua mahakimu na kuingilia kati maazimio ya kesi. Kama kesi inaangaliwa na serikali ni kawaida ya kwamba hukumu huamuliwa nje ya mahakama.
Polisi inapewa nafasi ya kuwatesa watu na hii ni aina ya adhabu bila sheria wala mahakama. Mara nyingi polisi zinapewa pia nafasi ya kuua watu hovyo au kuwafunga bila kesi kusikilizwa mahakamani.
Uchaguzi bandia
Utaratibu wa uchaguzi huru haufuatwi. Katika nchi kadhaa uchaguzi hufutwa kabisa kwa miaka mingi. Lakini mara nyingi kuna uchaguzi bandia badala ya uchaguzi huru. Kati ya njia mbalimbali za kuathiri matokeo ya uchaguzi ni:
kuteuliwa kwa wagombea na serikali na kukataliwa kwa wote ambao serikali haipendezwi nao.
mfumo wa chama kimoja ambamo viongozi wana nafasi ya kufukuza watu ambao hawapendezi katika chama na kuwatenga hivyo na siasa.
kutawala usimamizi wa uchaguzi na kutangaza matokeo kufuatana na mipango ya uongozi, si kutokana na kura zake ama uchaguzi hautokei au serikali inateua wagombea ikiondoa wapinzani wote au uchaguzi unaamuliwa awali na serikali ya kidikteta.
Uhuru wa maoni
Uhuru wa maoni unabanwa au hata kupigwa marufuku kabisa. Serikali inasimamia vyombo vya habari kama magazeti, redio na televisheni. Kutolewa kwa maoni yasiyopendwa na serikali ni kugumu. Hata hivyo kuna tofauti kwa sababu kuna udikteta ambako kuna kiwango fulani cha nafasi ya kupinga maazimio ya serikali kwenye ngazi za chini kwa mfano mjini au wilayani, hali za barabara au rushwa ya watumishi wadogo wa serikali. Lakini udikteta hauruhusu upinzani unaoendelea kueleza uhusiano kati ya makosa madogo na muundo wa serikali. Upinzani dhidi ya viongozi wa juu haukubaliwi.
Jambo la kawaida ni uteuzi wa habari zitakazoonekana kwenye vyombo vya habari. Nchi kadhaa zinajaribu pia kukataza habari za nje kufika. Katika Ujerumani ya Mashariki kwa miaka kadhaa antena za TV zilizoelekea magharibi zilipigwa marufuku kwa sababu serikali ilitaka kuzuia upatikanaji wa TV ya Ujerumani ya Magharibi. Katika Korea ya Kaskazini wananchi wa kawaida hawana nafasi ya kuangalia intaneti. China inatumia mitambo mingi inayojaribu kuzuia habari fulani kupitia intaneti; kuna programu ambazo zinazuia kuangalia kurasa zenye jina la “Dalai Lama” anayehofiwa kama mpinzani wa serikali.